Wednesday, March 18, 2015

VITA YA KAGERA: SIRI YA USHINDI WA TANZANIA

VITA YA KAGERA: SIRI YA USHINDI WA TANZANIA

Magari ya vita ya majeshi ya Idi Amini yakiwa kwenye formation kipindi cha vita ya Uganda

Na Gabriel Munyaga

Historia pengine haitatueleza moja kwa moja juu ya matukio yaliyopelekea kupiganwa kwa vita ya Kagera kati ya Uganda na Tanzania mnamo 1978-79. Utunzanji mbovu wa kumbukumbu na ukosefu wa wakereketwa wa kielimu juu ya tukio la Kagera kama mada ya uchambuzi wa kina wa kisomi katika elimu ya juu hapa nchini, unapelekea kutopatikana mada kinzani tofauti juu ya tukio hili la kihistoria. Katika kipindi ambacho kwa kasi ya taratibu tulikuwa tunakuza taifa pamoja na vyombo vyake vichanga, ikiwemo sekta ya habari, leo hii tunaona ni jinsi gani uwasilishwaji wa habari na hata propaganda juu ya vita ya Kagera uliongozwa na kiasi kikubwa kufanyika na vyombo vikubwa vya kimagharibi ambavyo vilikuwa vimeshajikita kwenye tasnia ya habari taarifa kwa miaka mingi.

Tunachoweza kupata leo, huku tukitingwa na muda na uwezekano wa kupata historia hii kutoka kwa washiriki wa vita hii, yaani maveterani wa vita ya Kagera, ni tafiti tu za habari tofauti tofauti kutoka vyanzo tofauti yakiwemo magazeti ya kale, vyanzo vya kimtandao na hata hadithi kwa wale walioishi kipindi cha vita hii, na kuunganisha tafiti hii yote na kujaribu kupata Makala moja yenye kugusa kila nyanja ya tukio hili.
Kwenye Makala yetu ya wiki iliyopita tuliangalia ni kwa jinsi gani upepo wa kisiasa pamoja na mgongano wa kimaslahi kati ya serikli nyingi za Afrika, ikiwemo Afrika ya Mashariki ulikuwa ni tishio kwa vitega uchumi na maslahi ya wakubwa wa magharibi na hivyo kuwa na mipangi mikakati ambayo ilitakiwa kufanya kazi pale tu mlengo wan chi flani ungekinzana na maslahi yao hapo, ama mategemeo yao kwa kiongozi flani yakaenda kinyume na kile kilichotazamiwa.

Katika Makala ile tuliona kuwa ni dhahiri Amini alipata msaada katika kuipindua serikali ya Milton Obote, msaada ambao kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na ulindaji wa maslahi ya bwana wa kikoloni wa Uganda. Na kwa kuwa changuo la Amini lilikwisha kuwapo tangu awali sana, na huku wakimjua na kukubali ya kuwa Amini ni mtu aliyekuwa na utaahira kidogo, ilihali wakamchagua kuwa ndiye kiongozi ambaye angefaa kulinda maslahi yao na ya Waganda, basi ni dhahili kuwa vita hii ingeweza kuepukika kwa kuchagua njia nyingine ya kutatua tatizo hili, mbali na kumuweka muuaji namba moja na kiongozi katili kabisa aliyewahi kushika madaraka Afrika.





Kati ya maswali tuliyoyauliza wiki iliyopita, mengi ni magumu kuyajibu kwa kufanya tafiti za kihabari mitandaoni ama kwa vyanzo vingine vya kijamii, lakini kinadharia tunaweza kujaribu. Kama tukijiuliza ya kuwa malengo ya muda mrefu ya kuwa na mshirika kama Amini yalikuwa ni yapi hasa, katika kipindi kile cha Afrika ya wakati ule ukilinganisha na ndoto ama mipango ya mbeleni ambayo serikali za mkoloni zilikuwa nazo kuhusu Afrika?

Kinadharia tunaweza kusema kuwa, serikali za mkoloni pengine hazikuwa na malengo chanya yoyote ya mbele kwa Afrika kwa takribani miaka ishirini mpaka ishirini na tano baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika. Baada ya kuona kuwa hazitaweza kuendeleza ukoloni, na kuwa fikra ya ukoloni kama mfumo wa kiuchumi na kiungozi hauwezi tena kufanya kazi, waliona kuwa kile ambacho wangeweza kufanya kwa kipindi hicho cha vuguvugu la uhuru mpka kupatiwa uhuru kwa nchi husika, ni kujaribu tu kulinda maslahi waliyoyaanzisha katika kipindi cha ukoloni kwa gharama yoyote ile, hata ikiwezekana kupindua serikali nzima iliyopo madarakani katika kufikia lengo hili. (Kama ilivyokuwa kwa Mohammed Mosadegh)

Nadharia hii inaweza kutiwa nguvu kwa kutazama mtitiriko wa matukio mengi ya Afrika changa kabisa, Afrika ya kipindi cha kijiongoza wenyewe. Madhumuni haya ya kudhani wangeweza kufikia malengo yao ya kimaslahi, yalitiwa nguvu na ukweli kwamba, uongozi wa Afrika ulikuwa unatoka katika mfumo wa kiasili, yaani mfumo wa Kifalme na Kichifu na kuingia mfumo wa Umma, ambapo mtu yeyote yule hata ambaye hakuwahi kupata mafunzo juu ya uongozi wa halaiki, kama ilivyokuwa kwa Amini, angeweza kuchukua hatamu za uongozi na baadaye kuwa mtii kwa mabwana zake wa kikoloni.

Lakini kama wasemavyo wazungu kuwa Power Corrupts na waswahili wasemavyo Pata Pesa(wakimaanisha nguvu) tujue tabia yako ndivyo ilivyotokea kwa viongozi hawa wa mwanzo, ukiwatoa wachache waliokuwa na njozi ya kweli.

Katika kuibukia siku za mwanzo za mgogoro wa Kagera, Watanzania chini ya Mwalimu walikuwa ni Wapweke kuliko walivyowahi kuwa hata siku nyingine. Maana anandika Dkt. Martin Luther King Jr kuwa ukimya wa rafiki zako unatisha zaidi kuliko kelele za adui. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Tanzania. Tukiangalia historia, katika ya manguli wa kisiasa na viongozi makini wa kipindii hicho, hakuna shaka kuwa Mwalimu alikuwa ni maridadi kabisa. Hawakumgwaya wenzake tu wa Afrika lakini hata wazungu waliheshimu akili yake inayochemka. Hatujui ni kwa nini waliaona kuwa Muswada wa Obote wa mlengo wa kijamaa, ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa ni nukushi ya azimio la Arusha, ulikuwa tishio kubwa sana kushinda Azimio la Arusha. Kwa sasa hayo tunaweza kuyaacha na tuangalie ni jinsi gani watanzania walipokea taarifa za uvamizi na ni kwa nini walishinda vita ya Kagera pamoja na changamoto zote zilizolikabiri jeshi la Tanzania kwa kipindi hicho.

Anaandika Bwana Attilio Tagalile kwenye Makala moja iliyotoka tarehe 14/10/2014 ya kuwa “Hatimaye yeyote yule atakaye kaa na kuandika historia ya vita ya Kagera,kazi yake hiyo haitakuwa timilifu kama haitaelezea ni kwa nini dunia nzima, pamoja na majirani wote wa Tanzania, walikataa kata kata kulaani kitendo Nduli Amini kuivamia Kagera, ijapokuwa Mwalimu Nyerere alitumia mwezi mmoja kuisihi jamii ya kimataifa pamoja na majirani zake kufanya hivyo.


Kitendo hichi hakikumshangaza Mwalimu tu peke yake bali kiliwachanganya Watanzania wote kwa ujumla. Amini ambaye tayari mpka kipindi cha uvamizi wa Kagera alikuwa na historia mbaya kabisa za ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini hakukemewa hata kwa maneno tu, si na mataifa ya magharibi ama jirani zetu Wakenya.

“hatuhitaji msaada waoo kumng’oa Amini, tunachotaka ni japo wao walaani tu kitendo hiki cha uvamizi, ni hicho tu’’ inasemekana aliwahi kunukuliwa Mwalimu akielezea juu ya ukimya wa jirani na marafiki zetu.

Kitendo hiki cha ukimya wa rafiki wa Watanzania na jirani pia ndio kilipelekea Mwalimu pamoja na makamanda wake wa vita kuamua kusonga mbele, sio tu kuikomboa Kagera, bali kumng’a nduli amini madarakani.

Ilichukua takribani wiki moja kwa majeshi ya Tanzania kumfukuza Amini Kagera, huku askari wake wakikimbia hovyo wasiamini kilichowatokea. Hadithi ya mkakati wa kuivamia Tanzania kupitia Kagera inakamilishwa na mpango wa jenerali Isaac Malyamungu ulijulikana kama opresheni Mugurusugu  ambao ulianza kama mazoezi ya kijeshi kati ya batalioni mbili, batalioni ya Simba iliyokuwa Mbarara na ile batalioni ya Gaddafi iliyokuwa Masaka.

Batalioni hizi mbili zikijifanya zipo mazoezini, zikaanza kurushiana risasi huku batalioni ya Masaka ikijifanya kukimbia risasi za wenzao na kuingia mpka Tanzania,. Huku wakiendelea na mazoezi hayo, batalioni ya Mbarara ikajifanya ikiwakimbiza mpaka Tanzania, na hivyo ndivyo walivamia na kukalia eneo hilo la Tanzania.

Ieleweke ya kuwa Uganda chini ya Idi Amini ilikuwa na washirika na marafiki wengi zaidi ambao walikuwa tayari kuitika pale tu Uganda ingewaita. Huku serikali ya Tanzania ikionekana kuwa mwiba kwa mataifa ya magharibi kwanza, kwa sera zake za ujamaa na kujitegemea zikifuatiwa na juhudi zake za kulikomboa bara la afrika dhidi ya wanyonyaji.

Waandishi wa habari wawili mme na mke walioruhusiwa na Mwalimu kufuatilia vita hii wakiwa mstari wa mbele, bwana Tony Avirgan na bibi Martha Honey wanasema kwenye kitabu chao kiitwacho War in Uganda: The Legacy of Idi Amini wanasema kuwa “Ni dhahiri kuwa sababu zilizofanya mataifa ya magharibi kumuunga mkono Amini juu ya uvamizi wa Kagera kwa namna moja ama nyingine ni sababu zile zile zilizowafanya wamuunge mkono juu ya mapinduzi ya Obote yaani siasa za kijamaa’’

Ni vizuri kutambua kuwa, kati ya miaka ya 1978 uchumi wa Tanzania ulikuwa ukikua vizuri japokuwa mwaka mmoja kabla iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika. Viwanda vingi vilivyokuwa upande wa Tanzania viliendelea kufanya vizuri. Yote hii pamoja na siasa ya ujamaa na kujitegemea ikijumlishwa na juhudi za Tanzania katika kulikomboa bara la Afrika hasa hasa kusini mwa Afrika, hakukuwafurahisha wakubwa wa magharibi. Na kati ya njia mojawapo ya kupunguza kasi ya Mwalimu katika juhudi yake hii ilikuwa ilikuwa ni kutengeneza matukio kaskazini mwa Tanzania, ili juhudi za ukombozi za kusini ziingie dosari.

Huku Mwalimu akiyajua yote haya, alicheza karata zake vizuri kwa kutotoa kauli tata wala kunyoosha kidole hata kwa wale rafiki zake. Bado akigubikwa na wingu zito la kutopata mshirika katika njia panda hii, ikiwamo iliyokuwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika, OAU. Huku Amini akifurahi kuungwa mkono na Saudi Arabia, chini ya Mfalme Faisal, PLO chini ya Yasser Arafat, Libya chini ya Muammar Gaddafi, Uingereza, Marekani kupitia CIA na Israel kabla ya kufunga uhusiano wake na nchini hiyo, bado Tanzania ilikuwa ikipanga mikakati peke yake. Hatimaye Tanzania ilipokea mkono wa msaada kutoka kwa raisi aliyekuwa mgonjwa kiasi cha kukata roho muda wowote ule. Raisi huyu si mwingine bali ni Kanali Houri Bomadiene wa Algeria aliyeacha usia kuwa, iwapo angekufa basi uongozi utakaofuata uisadie Tanzania kwa hali na mali kama vita itaibuka kati yake na Uganda.



  

Jinsi Tanzania ilivyoshinda vita ya Kagera ni hadithi ya kusisimua sana.pamoja na uchanga na kukosa washirika katika vita hii, bado jeshi la Tanzania liliweza kupata ushindi Kagera ndani ya takribani wiki moja tu.

Kati ya askari 45,000 waliopigana vita askari 15,000 ndio walitoka Jeshi la Wanachi la Tanzania. Huku wengine takribani 30,000 wakiwa ni wanamgambo ambao walipewa tu mafunzo ya haraka na kuruhusiwa kuingia vitani.

Inasemekana kuwa vijana hao walionyesha ushupavu mkubwa sana katika kupigana vita na kwa wale waliowaona katika upiganaji walisema kuwa, baada ya muda mfupi hukuweza kutofautisha mwanajeshi ni yupi na mwanamgambo ni yupi kwa kuwa wote walikuwa mahiri sana vitani.

Sababu nyingine ya kwa nini Tanzania ilishinda vita ilikuwa ni jinsi wanajeshi wa Tanzania walivyokuwa na maadili wakati wa vita. Badala ya kulenga raina na kuharibu mali zao, aksri kutoka Tanzania walilenga maficho ya adui pekee, tofauti na askari wa Amini ambao waliuwa raia na kuharibu na kuiba mali zao.

Kama askari wa Tanzania wangejiingiza katika vitendo vya mauaji ya raia, pengine ingekuwa ni vigumu sana kumaliza vita vile kwani raia wa Uganda wenyewe walisaidia kuonyesha walipojificha askari adui. Kauli ya kudumisha maadili ya vita ilisisitizwa na mwalimu kwa makamanda zake kipindi chote cha vita.
Hili lilijidhirisha ale mateka wa vita kutoka Libya na Palestina walikamatwa na baadae kurudishwa kwao wakiwa wanene kweli baada ya kulishwa na kutendewa haki kama mateka wa vita. Laiti isingekuwa sababu ya kudumisha maadili ya vita, ama War Ethics basi ingelikuwa ni shida kidogo kwa majeshi ya Tanzania kushinda vita hii.

Wakati tumegusia hapo mwanzo kuwa zaidi ya askari 30,000 walikuwa ni wanamgambo, na wachache ambao walikuwa na mafunzo ya juu waliwekwa akiba kama vita ingeendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja, Amini alikuwa akiuwa askari wake waliokuwa na mafunzo ya hali ya juu. Wakati vita inatokea, Amini alikuwa kapungukiwa kwa kiasi kikubwa na askari wake wenye mafunzo ya juu.

Tony Avirgan na Martha Honey wanasema kwenye kitabu chao “kama Amini angekuwa bado na jeshi alilolirithi kutoka kwa Obote, operesheni ya vita ya Kagera ingekuwa ngumu kidogo, kwani baada ya Kagera angeshuka mpaka Tabora na hapo ingekuwa ngumu kumtoa’’




Kama kuna kitu ambacho nchi za Afrika zilijifunza kutoka katika vita ya Kagera ni jinsi Mwalimu Nyerere alivyoendesha nchi, jeshi na diplomasia za kitaifa na Kimataifa. Ikiwa ya kuwa maswali mengi tunayojiuliza leo yanatokana na kusoma historia kama ilivyoandikwa, nab ado tunaibua walakaini, je hiyo ilikuwa kwa Mwalimu ambaye pamoja na kuwa mshirika namba moja wa ukombozi wa bara la Afrika hasa kusini mwa sahara, pamoja na kuwasilisha mfumo tofaut iwa kiuchumi ambao bado ilikuwa ni nadharia tu ambayo haukuwa na uhalisia wa vitendo, pamoja na undumilakuwili wa rafiki zake na jirani zake wakati wa shida, pamoja na kugeukwa na serikali ya Palestina aliyokuwa akiiunga mkono dhidi ya juu zao za ukombozi, lakini bado serikali hiyo hiyo ilituma askari ili wampindue, pamoja na juhudi za kuweka uongozi thabiti Uganda, Angola, Namibia, Mozambiquem Seychelles, Zimbambwe na hatimaye Afrika ya Kusini, pamoja na kuwa aliyafanya yote hayo akiwa peke yake, kwa kiasi kikubwa, bado mwalimu aliweza kuhakikisha usalama wa taifa lake, usalama wa mipaka ya Tanzania, usalama wa maish ayake pia na hata usalama wa Afrika kwa ujumla.
Ni dhahiri mwalimu alikuwa kurunzi ya matumaini kwa Afrika. Kiongozi aliyejari uhuru na kujitegemea dhidi ya ugaidi na umwagaji damu, haki dhidi ya udhalimu, Amani dhidi ya vita. Mwandishi mmoja alisema kuwa, ‘’Vile Tanzania leo hii inapoamua kuchukua muda kuyafikiria matakwa ama mapendekezo ya kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki, inapaswa iangaliwe historia pia, ni jinsi gani Tanzania ililipa bei ya kuweka matarajio yake yote mezani na kujikuta ikifanya mambo mengi peke yake ikiwemo vita ya Kagera’’

Anaandika Daniel G. Acheson-Brown katika tahariri yake katika kitivo cha Sayansi ya Kisiasa, Chuo kikuu cha Eastern New Mexico na kuuliza swali “Uvamizi wa Tanzania nchini Uganda: Je ni vita ya haki?

Nanukuu:

“Matumizi ya nguvu ya kijeshi ili kufikia malengo ya ukombozi wa binadamu kwa mwavuli wa sababu za haki yamekuwa ni mada yenye mguso sana tangu kipindi cha baada ya vita baridi. Hata hivyo, miaka kabla ya kuisha kwa vita baridi, Tanzania sio tu iliichapa Uganda na kurudisha ardhi iliyotekwa, bali iliendelea mpaka Uganda na kuung’a madarakani uongozi wa Amini. Lakini cha kushangaza, raisi Nyerere alikuwa kwenye njia panda tofauti sana na ile ya viongozi wa Ulaya na Marekani katika vita ya Ghuba, yaani kwamba, je? Kuacha vita baada ya malengo yaliyopangwa ya operesheni kutimia (Kama ilivyokuwa malengo ya kuiomboa Kagera), ama kuendeleza operesheni mbele zaidi na kumng’oa kiongozi dhalimu? Na kwa sababu Nyerere aliamua kuendelea na kumng’oa kiongozi dhalimu, ilimpasa pia afikirie maamuzi yake katika kuijenga upya Uganda na sehemu yake ya uongozi, kwani msingi wa kutumia nguvu ya jeshi kwa matumizi ya ukombozi wa watu, umesimikwa kwenye maadili’’

Email: gabby.munyaga@gmail.com
Facebook: Gabriel Munyaga
Twitter: GabrielMunyaga
Blog: gabbymunyaga.blogspot.com  





No comments:

Post a Comment