VITA YA KAGERA: JINSI SERIKALI ZA MAGHARIBI
ZINGEWEZA KUIZUIA
Kundi la askari wa NRA wakipiga
kwata huku ndege vita aina ya P-40 Warhawk ikipita juu
Na Gabriel Munyaga
Tukijikumbusha matukio yaliyojiri katika vita ya
Kagera, wengi wetu tunaweza kunyooshea kidole kitendo kile cha Idi Amini
kuvamia sehemu ya Tanzania, na baadaye serikali ya Tanzania chini ya Raisi
Julius Nyerere kuamua kujibu mashambulizi ili kumfukuza nduli Amini na hatimaye
kumtoa kabisa madarakani.
Lakini kwa wachambuzi wa kina wa mambo, tatizo la
nduli Amini halikuanzia tu miaka ya 1971 kipindi alichompindua Raisi aliyekuwa
madarakani, Daktari Milton Obote. Lakini matatizo ya Amini kama chaguo la pili
la serikali za magharibi iwapo tu ingetokea kutokuelewana na uongozi uliokuwapo
kwa kipindi kile, yaani wa Milton Obote, yalishapangwa na serikali hizi tangu
hata kabla ya Uhuru wa Uganda, na kuna wanaosema kuwa Serikali za Magharibi
zilijua, ama kwa sehemu fulani pia zilisaidia mapinduzi ya Obote na Amin
kujinyakulia madaraka. Hebu tuangalie historia ya vita hivi ambayo iliiacha
Tanzania katika wakati mgumu sana kifedha.
Idi Amin alijiunga na jeshi la mkoloni mnamo miaka
ya 1946 akipangiwa kufanya kazi Kenya, Uganda na Somalia na mnamo miaka ya 1950
alitumika katika operesheni ya kudhoofisha makundi ya kudai uhuru huko Kenya.
Makala moja mtandaoni inasema kuwa, ‘’kisichojulikana kwa wazi sana ni jinsi
gani Serikali ya Uingereza ilivyofanya kazi sio tu kuzuia ukatili wa Amini,
bali hata kumuweka madarakani.’’
Hadithi ya ni jinsi gani madola ya magharibi
yalitumia mbinu ili kulinda mali na utajiri wao uliokuwa unaporomoka kipindi
cha miaka ya 1960 ni ndefu na ya kuchanganya, lakini yaonekana kilichokuwa kinawatisha
zaidi sio tu Waafrika waliokuwa wakidai uhuru wao kwa nguvu, na ni jinsi gani
wawache watawale, bali ni fikra, dhana na mifumo ya serikali ambayo viongozi
hawa wangeitumia kuongezea Afrika baada ya wao kuachia ngazi.
Japokuwa hata serikali ya Milton Obote nayo
iligubikwa na uonevu na ukiukwaji wa haki za binadmu, hilo halikuwatisha sana
wazungu lakini pale alipoonyesha dalili za kuegemea siasa za ujamaa na
ubinafsishaji wa mali binafsi kuwa za umma, hapo ndipo kazi ilipoanza.
Mnamo mwaka 1969-70 Obote alitoa machapisho yake
yaliyojulikana kama The Common Man’s
Charter ambayo ulielezea dhamira yake ya kuegemea kwenye mfumo wa kijamaa
na sera za mlengo wa kushoto ambapo serikali ilijichukulia umiliki hadi wa
asilimia 60 kwenye mabenki yote binafsi pamoja na mashirika binafsi, na kufanya
biashara hizi zisimamiwe na serikali. Hilo lilipelekea kushamiri vitendo vya
rushwa isiyoelezeka.
Kuvurugwa huku kwa uchumi kulipelekea bei za vyakula
kupanda juu na bidhaa na mahitajii muhimu kukosekana, na zaidi zaidi kitendo
cha raisi Obote kuwafunga jela wafanyabiashara wenye asili ya kihindi
kuliongeza ukosekanaji wa bidhaa masokoni.
Kwa upande mwingine, sera hii ya ujamaa na
ubinafsishaji, ilitishia maslahi ya uingereza ambayo ilikuwa na makampuni 80
makubwa nchini humo. Milki hii ya viwanda na mabiashara makubwa yote yalikuwa
mashakani kutokana na sera ya bwana Obote. Kwa kuwa alikuwa na ukaribu na
serikali za Israel, Marekani na Uingereza, Obote alikubali msaada wa kifedha
kutoka Israel, ambayo kipindi hicho ilikuwa inapigania kuwa na washirika wake
Afrika na kwingineko duniani, huku ikitumiwa na Marekani kuwa mstari wa mbele
katika sehemu zile ambazo Marekani haikuwa na sura nzuri sana.
Nchi hizi zote zilifanya kazi kwa ukaribu hapo
Uganda kupitia mashirika yao ya ujasusi, yakiwemo CIA na Mossad. Huku
Washington ikitoa fedha za msaada za maendeleo, Israel ilitoa mafunzo kwa jeshi
la ardhi na jeshi anga la Uganda, huku uwepo wa kibiashara na kisiasa wa
Uingereza ukiwa kila mahali. Jambo hili lilimtatiza Obote na alipanga
kulibadili kwa kufanya mabadiliko ya kisheria juu ya hali hiyo, ambayo ni
dhhiri yangetingisha misingi ya maslahi ya serikali hizo za kikoloni.
Mchangiaji mmoja anasema kuwa ‘’Japokuwa Obote
hakuwa Fidel Castro ama Julius Nyerere, muswada wake uliojulikana kama Common
Man’s Charter na ubinafsishaji wa makampuni 80 ya Uingereza, haukupokelewa
vizuri huko London, kwani Serikali ya Obote ilikuwa ipo mbioni na karibu
kabisa, sio kubadili katiba ya Uganda,
bali mfumo mzima wa kisiasa.
Kutokana na ukaribu wa Marekani, Uingereza na Israel
nchini Uganda, pamoja na mafunzo ya kijeshi na program za misaada zilizokuwa
zikifanywa nan chi hizo, walianza kufanya mikakati ya kusawazisha hali hiyo. Na
kitu cha kwanza ilikuwa ni kumtafuta mrithi wa Obote, na Amini alionekana kuwa
ni chaguo lisilopingika. Amini aliyejulikana kwa Waingereza kama taahira
kidogo, lakini mtu mtiifu sana kwa Uingereza, yasemekana alianza kuandaliwa
kuwa mrithi wa Obote tangu miaka ya 1966, ikiwa ni miaka minne tu tangu Uganda
ipate uhuru, lakini mikakati hasa ya kumuingiza madarakani ilianza mwaka 1969,
huko kusini mwa Sudan na kipindi ambacho Obote alianza kampeni zake za
ubinafsishaji.
Katika eneo hilo la Sudan ya kusini, majasusi wa
shirika ujasusi la Isarael Mossad, walikuwa kwenye vijiji ambavyo vilikuwa
tiifu kwa Amin, kwani alikuwa ni wa asili yao, ambapo walikuwa wakiunga mkono
na kusaidia vugu vugu la kujitenga la makundi yaliyojulikana kama Anya-nya
dhidi ya Serikali ya Sudan ambayo inaunga mkono mataifa ya kiarabu.
Lengo la Mossad kusaidia kundi hilo lenye vugu vugu
ya kujitenga ilikuwa ni kurubuni Serikali ya Sudan kutoa majeshi yake mbali na
mpaka wa magharibi wa Misri na kuyaleta huku kwenye machafuko, ili kupunguza
idadi ya majeshi yanayounga mkono nchi za kiarabu katika mpaka wake na Misri.
Inasemekana kuwa, siku chache kabla ya mapinduzi ya
kijeshi ya Idi Amin, askari wapatao 700 wa jeshi la Uingereza waliwasili nchini
Kenya. Serikali ya Uingereza ilijitetea kuwa askari hao watatumika tu kama
vurugu zingetokea dhidi ya waingereza na dhidi ya maslahi ya Uingereza kipindi
Uingereza iliposimamia suala lake la kuiuzia Afrika Kusini ya mkaburu silaha.
Ijulikane kuwa, katika kipindi hicho hicho, serikali ya Uingereza ikiongozwa na
Waziri Mkuu Edward Heath ilishikilia bango hatua yake ya kuiuzia silaha Afrika
ya Kusini ya makaburu, kitendo ambacho kilipingwa sana na nchi wanachama wa
Jumuiya ya Madola, ikiwemo Tanzania.
Huku mikakati ya kumuondoa Obote ikiwa imepamba
moto, kukatokea kikao cha nchi washirika wa Jumuiya ya Madola, kilichofanyika
Singapore mnamo mwaka wa 1971. Mada kubwa ilikuwa ni kitendo cha Uingereza
kuiuzia Afrika ya Kusini ya mkaburu silaha ambazo zingeenda kuua na kuendeleza
ukandamizaji wa wengi dhidi ya wachache.
Inasemekana kuwa Rais Nyerere alimsihi Obote waende
wote Singapore kwenye kikao hicho cha Jumuiya ya Madola, ili kutia nguvu zaidi
katika kuishinikiza serikaliya Uingereza kusitisha mpango wake huo. Huku
wakindelea na mkutano, nyumbani Amin alipindua nchi.
Yasemekana kuwa katika kikao cha faragha kati ya
Raisi Kaunda, Mwalimu Nyerere na Milton Obote walichofanya na Waziri Mkuu huyo
wa bwana Edward Heath, walitishia kujitoa katika Jumuiya hiyo ya Madola kama tu
Uingereza ingeendelea na msimamo wake wa kuuzia sila Afrika Kusini ya mkaburu, bwana
Heath aliwatazama na kuwaambia ‘’ sijui wangapi kati yenu mtaruhusiwa kurudi
nchini mwenu baada ya mkutano huu’’
Baada ya kunyakua madaraka, Serikali ya Uingereza
ikawa kati ya Serikali za kwnza kabisa kuutambua uongozi wa Uganda chini ya
Amin, huku vyombo vya habari vya Uingereza vikimpongeza na hata kuwabeza akina
Obote na Kaunda ya kuwa wanapenda sifa tu a kimataifa na si kazi ya kuendesha
nchi. Huku marekani ikisita moja kwa moja kuitambua serikali ya Amin, lakini
pia ilishangazwa na uharaka waSerikali ya Uingereza kumtambua Amin moja kwa
moja.
Amin alianza vizuri akiwa mtiifu kwa mataifa ya
magharibi. Kwanza alimuunga mkono waziri mkuu Edard Heath katika uuzaji wa
silaha kwa Afrika kusini ya mkaburu, na hivyo kuvunja nadhiri waliyoweka
Kaunda, Obote na Nyerere. Pili alirudisha kwa Uingereza baadhi ya makampuni
yaliyobinafsishwa chini ya Obote na miezi sita baada ya mapinduzi alialikwa Uingereza
na kula chakula cha mchana na Malkia, huku akipata wasaa wa kukutana na baraza
la mawaziri chini ya bwana Heath.
Lakini kama wasemavyo waswahili, pata madaraka tujue
tabia yako, ndivyo hali ilivyoanza kuwa tofauti nkwa Amin na washirika zake.
Mara tu baada ya mapinduzi, Amin alipewa kiasi cha Paundi Milioni 10 za
Uingereza kama msaada pamoja na magari 15 yasiyopita risasi aina ya Ferret na
mengine 36 aina ya Saladin.
Gari ya vita ina ya Ferret
Kitendo hiki kilimchukiza Amin kwani yeye alikuwa
anataka ndege-vita ili kutimiza malengo yake ya kiutanuzi dhidi ya Tanzania,
kwa kutaka kujimegea kipande cha kutoka Kagera mpka Tanga ilia pate bandari nay
eye katika pwani ya mashariki.
Lakini pia tayari vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binadamu viliendelea kushamiri sana nchini Uganda na wanajeshi wengi na raia
pamoja na wanasiasa, walikuwa wakikimbilia Tanzania kutafuta hifadhi ya
kisiasa. Hivyo baada ya Amin kunyimwa ndege-vita na Waingereza, akawageukia
Waisrael na kuomba ndege vita aina ya Phantom. Israel isingeweza kutoa maamuzi
kama hayo peke yake bila ruhusa ya Marekani lakini napo alinyimwa sababu ikitajwa
kuwa, maombo hayo yanapitiliza matakwa ya kiulinzi ya kiuhalisia, yaani hakuwa
na tishio la kuvamiwa kokote. Kwa hasira akafukuza Wayahudi wote waliokuwa
Uganda.
Huku akiona ndoto yake ikififia na anakosa vifaa
madhubuti vya kivita, aligeukia ushauri wa kifikra na kimkakati kutoka kwa
mwanajeshi mmoja aliyestaafu wa Uingereza aliyekuwa anakaa pembezoni mwa mto
Kagera mpakani mwa uganda na Tanzania.
Inasemekana mwanajeshi huyo kwa kiasi kikubwa
alimsaidia Amin kimkakati, kiintelijenstia na kiushauri juu ya mpango wake wa
kuivamia Tanzania na kumega kipande cha ardhi. Lakini kwa kipindi chote hicho
baada ya serikali kadhaa kusitisha mahusiano na Uganda, Uingereza bado
haikusitisha mahusiano na Uganda. Inasemekana kuwa, baada ya uchumi kuporomoka
na chakula kuanza kugaiwa kwa mgao, chakula cha Amin pamoja na washirika wake,
wakiwamo makamanda wa juu wa jeshi la Uganda, walikuwa wanapatiwa chakula
kutoka Uingereza kupitia uwanja wa ndege wa Stansted, huko Essex.
Baada ya mikakati yake ya kuivamia Tanzania kuiva,
pamoja na ushauri aliokuwa anaupata kutoka kwamwanajeshi huyo mstaafu, Amin
alijithibitishia uwezo wake wa kuivamia Tanzania. Mpaka leo haijulikani kama
mwanajeshi huyo mstaafu alikuwa anafanya kazi kwa amri kutoka London ama
alikuwa kivyake, lakini upo uthibitisho kuwa alikuwa bado ana mawasiliano na
serikali ya London. Ni mwanajeshi huyo aliyemsaidia Amin na kumpamba moto
kuhusu mkakati wake wa kuivamia Tanzania.
Huku tukiwa hatujui hatima ya wale askari 700 wa
Uingereza waliotua Kenya kabla ya mapinduzi, kuna wanaosema kuwa, baada ya
Uingereza kuona kuwa Amin sasa amekuwa mzigo, kwa namna moja au nyingine iliona
kuwa njia rahisi ya kumuondoa madarakani ni kupitia jirani yake.
Na hatimaye mnamo mwaka wa 1978, Idi Amin aliivamia
Tanzania, na hilo likapelekea Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya wanainchi wa
Tanzania, kutangaza vita rasmi na nduli Amin, na kuruhusu vikosi vikamwondoe adui
huyu siyo tu Kagera, lakini mpaka Kampala.
Tanzania iliweza kupata magari ya kurusha makombora
ya Kisoviet, yajulikanayo kama BM Katyusha, ambayo waliyatumia ipasavyo katika
kuvurumusha makombora dhidi ya askari wa Amin.
Amin alipata washirika wa vita dhisi ya Tanzania.
Nao walikuwa ni Muammar Gaddafi wa Libya na Yasser Arafat wa Palestinian
Liberation Organization. Muammar Gaddafi aliipatia Uganda askari wake takribani
3000 na Palestina ilitoa askari 200 na ushee. Uganda yenyewe ilianza vita na
askri 70,000 huku Tanzania ikianza na askari 40,000 tu, lakini baadaye Serikali
ikabidi ichukue askari kutoka vyombo vingine vya ulinzi kama Polisi, Askari
Magereza na hata Wanamgambo.
Hata hivyo askari wengi wa Libya walijikuta wapo
mstari wa mbele wa mapambano, badala ya askari wa Uganda, kwani wao walikuwa
wakihangaikia ni jinsi gani watasafirisha mali walizoiba kwa wananchi, kwenye
kipindi hicho cha vita. Wakawa wanatumia magari ya jeshi kubebea mali za wizi
badala ya kushugulika na vita.
Ingawa Tanzania ilipoteza askari wake 373 na raia
karibia 1500, iliibuka mshindi kwenye vita hii ambayo kwa ujumla ilikuwa ni
vita ya Amin peke yake na uroho wake wa mali na madaraka.
Ingawa Amin alifanikiwa kutorokea Libya na baadaye
mpaka Saudi Arabia, tukiangalia matukio ya mwisho ya kiongozi huyu, tunabaki na
maswali lukuki kichwani.
Baadhi tu ni je? Kuingia kwake madarakani kweli kwa
kiasi fulani kulichangiwa na dola kubwa hapa duniani? Je ni nini yalikuwa
malengo ya kuwa na mshirika kama Amin, malengo ya muda mrefu yalikuwa ni yapi
hasa. Haya na mengine tutayaangalia kwa kina katika muendelezo wa Makala hii wiki ijayo.
Itaendelea wiki ijayo
Facebook: Gabriel Munyaga
Twitter: GabrielMunyaga
No comments:
Post a Comment