VITA YA KAGERA: SIRI YA USHINDI WA TANZANIA
Magari ya vita ya majeshi ya Idi Amini yakiwa kwenye
formation kipindi cha vita ya Uganda
Na Gabriel Munyaga
Historia pengine haitatueleza moja
kwa moja juu ya matukio yaliyopelekea kupiganwa kwa vita ya Kagera kati ya
Uganda na Tanzania mnamo 1978-79. Utunzanji mbovu wa kumbukumbu na ukosefu wa
wakereketwa wa kielimu juu ya tukio la Kagera kama mada ya uchambuzi wa kina wa
kisomi katika elimu ya juu hapa nchini, unapelekea kutopatikana mada kinzani
tofauti juu ya tukio hili la kihistoria. Katika kipindi ambacho kwa kasi ya
taratibu tulikuwa tunakuza taifa pamoja na vyombo vyake vichanga, ikiwemo sekta
ya habari, leo hii tunaona ni jinsi gani uwasilishwaji wa habari na hata
propaganda juu ya vita ya Kagera uliongozwa na kiasi kikubwa kufanyika na
vyombo vikubwa vya kimagharibi ambavyo vilikuwa vimeshajikita kwenye tasnia ya
habari taarifa kwa miaka mingi.
Tunachoweza kupata leo, huku
tukitingwa na muda na uwezekano wa kupata historia hii kutoka kwa washiriki wa
vita hii, yaani maveterani wa vita ya Kagera, ni tafiti tu za habari tofauti
tofauti kutoka vyanzo tofauti yakiwemo magazeti ya kale, vyanzo vya kimtandao
na hata hadithi kwa wale walioishi kipindi cha vita hii, na kuunganisha tafiti
hii yote na kujaribu kupata Makala moja yenye kugusa kila nyanja ya tukio hili.
Kwenye Makala yetu ya wiki iliyopita
tuliangalia ni kwa jinsi gani upepo wa kisiasa pamoja na mgongano wa kimaslahi
kati ya serikli nyingi za Afrika, ikiwemo Afrika ya Mashariki ulikuwa ni tishio
kwa vitega uchumi na maslahi ya wakubwa wa magharibi na hivyo kuwa na mipangi
mikakati ambayo ilitakiwa kufanya kazi pale tu mlengo wan chi flani ungekinzana
na maslahi yao hapo, ama mategemeo yao kwa kiongozi flani yakaenda kinyume na
kile kilichotazamiwa.
Katika Makala ile tuliona kuwa ni
dhahiri Amini alipata msaada katika kuipindua serikali ya Milton Obote, msaada
ambao kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na ulindaji wa maslahi ya bwana wa kikoloni
wa Uganda. Na kwa kuwa changuo la Amini lilikwisha kuwapo tangu awali sana, na
huku wakimjua na kukubali ya kuwa Amini ni mtu aliyekuwa na utaahira kidogo,
ilihali wakamchagua kuwa ndiye kiongozi ambaye angefaa kulinda maslahi yao na ya
Waganda, basi ni dhahili kuwa vita hii ingeweza kuepukika kwa kuchagua njia
nyingine ya kutatua tatizo hili, mbali na kumuweka muuaji namba moja na
kiongozi katili kabisa aliyewahi kushika madaraka Afrika.
Kati ya maswali tuliyoyauliza wiki iliyopita,
mengi ni magumu kuyajibu kwa kufanya tafiti za kihabari mitandaoni ama kwa
vyanzo vingine vya kijamii, lakini kinadharia tunaweza kujaribu. Kama tukijiuliza
ya kuwa malengo ya muda mrefu ya kuwa na mshirika kama Amini yalikuwa ni yapi hasa,
katika kipindi kile cha Afrika ya wakati ule ukilinganisha na ndoto ama mipango
ya mbeleni ambayo serikali za mkoloni zilikuwa nazo kuhusu Afrika?
Kinadharia tunaweza kusema kuwa,
serikali za mkoloni pengine hazikuwa na malengo chanya yoyote ya mbele kwa
Afrika kwa takribani miaka ishirini mpaka ishirini na tano baada ya uhuru wa nchi
nyingi za Afrika. Baada ya kuona kuwa hazitaweza kuendeleza ukoloni, na kuwa
fikra ya ukoloni kama mfumo wa kiuchumi na kiungozi hauwezi tena kufanya kazi,
waliona kuwa kile ambacho wangeweza kufanya kwa kipindi hicho cha vuguvugu la
uhuru mpka kupatiwa uhuru kwa nchi husika, ni kujaribu tu kulinda maslahi
waliyoyaanzisha katika kipindi cha ukoloni kwa gharama yoyote ile, hata ikiwezekana
kupindua serikali nzima iliyopo madarakani katika kufikia lengo hili. (Kama
ilivyokuwa kwa Mohammed Mosadegh)
Nadharia hii inaweza kutiwa nguvu kwa
kutazama mtitiriko wa matukio mengi ya Afrika changa kabisa, Afrika ya kipindi
cha kijiongoza wenyewe. Madhumuni haya ya kudhani wangeweza kufikia malengo yao
ya kimaslahi, yalitiwa nguvu na ukweli kwamba, uongozi wa Afrika ulikuwa
unatoka katika mfumo wa kiasili, yaani mfumo wa Kifalme na Kichifu na kuingia
mfumo wa Umma, ambapo mtu yeyote yule hata ambaye hakuwahi kupata mafunzo juu
ya uongozi wa halaiki, kama ilivyokuwa kwa Amini, angeweza kuchukua hatamu za
uongozi na baadaye kuwa mtii kwa mabwana zake wa kikoloni.
Lakini kama wasemavyo wazungu kuwa Power Corrupts na waswahili wasemavyo Pata Pesa(wakimaanisha nguvu) tujue tabia
yako ndivyo ilivyotokea kwa viongozi hawa wa mwanzo, ukiwatoa wachache
waliokuwa na njozi ya kweli.
Katika kuibukia siku za mwanzo za mgogoro
wa Kagera, Watanzania chini ya Mwalimu walikuwa ni Wapweke kuliko walivyowahi
kuwa hata siku nyingine. Maana anandika Dkt. Martin Luther King Jr kuwa ukimya
wa rafiki zako unatisha zaidi kuliko kelele za adui. Hivyo ndivyo ilivyokuwa
kwa Tanzania. Tukiangalia historia, katika ya manguli wa kisiasa na viongozi
makini wa kipindii hicho, hakuna shaka kuwa Mwalimu alikuwa ni maridadi kabisa.
Hawakumgwaya wenzake tu wa Afrika lakini hata wazungu waliheshimu akili yake
inayochemka. Hatujui ni kwa nini waliaona kuwa Muswada wa Obote wa mlengo wa
kijamaa, ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa ni nukushi ya azimio la Arusha,
ulikuwa tishio kubwa sana kushinda Azimio la Arusha. Kwa sasa hayo tunaweza
kuyaacha na tuangalie ni jinsi gani watanzania walipokea taarifa za uvamizi na
ni kwa nini walishinda vita ya Kagera pamoja na changamoto zote zilizolikabiri
jeshi la Tanzania kwa kipindi hicho.
Anaandika Bwana Attilio Tagalile
kwenye Makala moja iliyotoka tarehe 14/10/2014 ya kuwa “Hatimaye yeyote yule
atakaye kaa na kuandika historia ya vita ya Kagera,kazi yake hiyo haitakuwa
timilifu kama haitaelezea ni kwa nini dunia nzima, pamoja na majirani wote wa
Tanzania, walikataa kata kata kulaani kitendo Nduli Amini kuivamia Kagera,
ijapokuwa Mwalimu Nyerere alitumia mwezi mmoja kuisihi jamii ya kimataifa
pamoja na majirani zake kufanya hivyo.
Kitendo hichi hakikumshangaza Mwalimu
tu peke yake bali kiliwachanganya Watanzania wote kwa ujumla. Amini ambaye
tayari mpka kipindi cha uvamizi wa Kagera alikuwa na historia mbaya kabisa za
ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini hakukemewa hata kwa maneno tu, si na
mataifa ya magharibi ama jirani zetu Wakenya.
“hatuhitaji msaada waoo kumng’oa
Amini, tunachotaka ni japo wao walaani tu kitendo hiki cha uvamizi, ni hicho tu’’
inasemekana aliwahi kunukuliwa Mwalimu akielezea juu ya ukimya wa jirani na
marafiki zetu.
Kitendo hiki cha ukimya wa rafiki wa
Watanzania na jirani pia ndio kilipelekea Mwalimu pamoja na makamanda wake wa
vita kuamua kusonga mbele, sio tu kuikomboa Kagera, bali kumng’a nduli amini
madarakani.
Ilichukua takribani wiki moja kwa
majeshi ya Tanzania kumfukuza Amini Kagera, huku askari wake wakikimbia hovyo
wasiamini kilichowatokea. Hadithi ya mkakati wa kuivamia Tanzania kupitia Kagera
inakamilishwa na mpango wa jenerali Isaac Malyamungu ulijulikana kama opresheni
Mugurusugu ambao ulianza kama mazoezi ya
kijeshi kati ya batalioni mbili, batalioni ya Simba iliyokuwa Mbarara na ile batalioni
ya Gaddafi iliyokuwa Masaka.
Batalioni hizi mbili zikijifanya zipo
mazoezini, zikaanza kurushiana risasi huku batalioni ya Masaka ikijifanya
kukimbia risasi za wenzao na kuingia mpka Tanzania,. Huku wakiendelea na
mazoezi hayo, batalioni ya Mbarara ikajifanya ikiwakimbiza mpaka Tanzania, na
hivyo ndivyo walivamia na kukalia eneo hilo la Tanzania.
Ieleweke ya kuwa Uganda chini ya Idi
Amini ilikuwa na washirika na marafiki wengi zaidi ambao walikuwa tayari
kuitika pale tu Uganda ingewaita. Huku serikali ya Tanzania ikionekana kuwa
mwiba kwa mataifa ya magharibi kwanza, kwa sera zake za ujamaa na kujitegemea
zikifuatiwa na juhudi zake za kulikomboa bara la afrika dhidi ya wanyonyaji.
Waandishi wa habari wawili mme na mke
walioruhusiwa na Mwalimu kufuatilia vita hii wakiwa mstari wa mbele, bwana Tony
Avirgan na bibi Martha Honey wanasema kwenye kitabu chao kiitwacho War in Uganda: The Legacy of Idi Amini wanasema
kuwa “Ni dhahiri kuwa sababu zilizofanya mataifa ya magharibi kumuunga mkono
Amini juu ya uvamizi wa Kagera kwa namna moja ama nyingine ni sababu zile zile
zilizowafanya wamuunge mkono juu ya mapinduzi ya Obote yaani siasa za kijamaa’’
Ni vizuri kutambua kuwa, kati ya
miaka ya 1978 uchumi wa Tanzania ulikuwa ukikua vizuri japokuwa mwaka mmoja
kabla iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika. Viwanda vingi
vilivyokuwa upande wa Tanzania viliendelea kufanya vizuri. Yote hii pamoja na
siasa ya ujamaa na kujitegemea ikijumlishwa na juhudi za Tanzania katika
kulikomboa bara la Afrika hasa hasa kusini mwa Afrika, hakukuwafurahisha
wakubwa wa magharibi. Na kati ya njia mojawapo ya kupunguza kasi ya Mwalimu
katika juhudi yake hii ilikuwa ilikuwa ni kutengeneza matukio kaskazini mwa
Tanzania, ili juhudi za ukombozi za kusini ziingie dosari.
Huku Mwalimu akiyajua yote haya,
alicheza karata zake vizuri kwa kutotoa kauli tata wala kunyoosha kidole hata
kwa wale rafiki zake. Bado akigubikwa na wingu zito la kutopata mshirika katika
njia panda hii, ikiwamo iliyokuwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika, OAU. Huku Amini
akifurahi kuungwa mkono na Saudi Arabia, chini ya Mfalme Faisal, PLO chini ya
Yasser Arafat, Libya chini ya Muammar Gaddafi, Uingereza, Marekani kupitia CIA
na Israel kabla ya kufunga uhusiano wake na nchini hiyo, bado Tanzania ilikuwa
ikipanga mikakati peke yake. Hatimaye Tanzania ilipokea mkono wa msaada kutoka
kwa raisi aliyekuwa mgonjwa kiasi cha kukata roho muda wowote ule. Raisi huyu
si mwingine bali ni Kanali Houri Bomadiene wa Algeria aliyeacha usia kuwa,
iwapo angekufa basi uongozi utakaofuata uisadie Tanzania kwa hali na mali kama
vita itaibuka kati yake na Uganda.
Jinsi Tanzania ilivyoshinda vita ya
Kagera ni hadithi ya kusisimua sana.pamoja na uchanga na kukosa washirika
katika vita hii, bado jeshi la Tanzania liliweza kupata ushindi Kagera ndani ya
takribani wiki moja tu.
Kati ya askari 45,000 waliopigana vita
askari 15,000 ndio walitoka Jeshi la Wanachi la Tanzania. Huku wengine
takribani 30,000 wakiwa ni wanamgambo ambao walipewa tu mafunzo ya haraka na
kuruhusiwa kuingia vitani.
Inasemekana kuwa vijana hao
walionyesha ushupavu mkubwa sana katika kupigana vita na kwa wale waliowaona
katika upiganaji walisema kuwa, baada ya muda mfupi hukuweza kutofautisha
mwanajeshi ni yupi na mwanamgambo ni yupi kwa kuwa wote walikuwa mahiri sana
vitani.
Sababu nyingine ya kwa nini Tanzania ilishinda
vita ilikuwa ni jinsi wanajeshi wa Tanzania walivyokuwa na maadili wakati wa
vita. Badala ya kulenga raina na kuharibu mali zao, aksri kutoka Tanzania walilenga
maficho ya adui pekee, tofauti na askari wa Amini ambao waliuwa raia na
kuharibu na kuiba mali zao.
Kama askari wa Tanzania wangejiingiza
katika vitendo vya mauaji ya raia, pengine ingekuwa ni vigumu sana kumaliza
vita vile kwani raia wa Uganda wenyewe walisaidia kuonyesha walipojificha
askari adui. Kauli ya kudumisha maadili ya vita ilisisitizwa na mwalimu kwa
makamanda zake kipindi chote cha vita.
Hili lilijidhirisha ale mateka wa
vita kutoka Libya na Palestina walikamatwa na baadae kurudishwa kwao wakiwa
wanene kweli baada ya kulishwa na kutendewa haki kama mateka wa vita. Laiti
isingekuwa sababu ya kudumisha maadili ya vita, ama War Ethics basi ingelikuwa ni shida kidogo kwa majeshi ya Tanzania
kushinda vita hii.
Wakati tumegusia hapo mwanzo kuwa
zaidi ya askari 30,000 walikuwa ni wanamgambo, na wachache ambao walikuwa na
mafunzo ya juu waliwekwa akiba kama vita ingeendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja, Amini
alikuwa akiuwa askari wake waliokuwa na mafunzo ya hali ya juu. Wakati vita
inatokea, Amini alikuwa kapungukiwa kwa kiasi kikubwa na askari wake wenye
mafunzo ya juu.
Tony Avirgan na Martha Honey wanasema
kwenye kitabu chao “kama Amini angekuwa bado na jeshi alilolirithi kutoka kwa
Obote, operesheni ya vita ya Kagera ingekuwa ngumu kidogo, kwani baada ya
Kagera angeshuka mpaka Tabora na hapo ingekuwa ngumu kumtoa’’
Kama kuna kitu ambacho nchi za Afrika
zilijifunza kutoka katika vita ya Kagera ni jinsi Mwalimu Nyerere alivyoendesha
nchi, jeshi na diplomasia za kitaifa na Kimataifa. Ikiwa ya kuwa maswali mengi
tunayojiuliza leo yanatokana na kusoma historia kama ilivyoandikwa, nab ado tunaibua
walakaini, je hiyo ilikuwa kwa Mwalimu ambaye pamoja na kuwa mshirika namba
moja wa ukombozi wa bara la Afrika hasa kusini mwa sahara, pamoja na
kuwasilisha mfumo tofaut iwa kiuchumi ambao bado ilikuwa ni nadharia tu ambayo
haukuwa na uhalisia wa vitendo, pamoja na undumilakuwili wa rafiki zake na
jirani zake wakati wa shida, pamoja na kugeukwa na serikali ya Palestina
aliyokuwa akiiunga mkono dhidi ya juu zao za ukombozi, lakini bado serikali
hiyo hiyo ilituma askari ili wampindue, pamoja na juhudi za kuweka uongozi
thabiti Uganda, Angola, Namibia, Mozambiquem Seychelles, Zimbambwe na hatimaye
Afrika ya Kusini, pamoja na kuwa aliyafanya yote hayo akiwa peke yake, kwa
kiasi kikubwa, bado mwalimu aliweza kuhakikisha usalama wa taifa lake, usalama
wa mipaka ya Tanzania, usalama wa maish ayake pia na hata usalama wa Afrika kwa
ujumla.
Ni dhahiri mwalimu alikuwa kurunzi ya
matumaini kwa Afrika. Kiongozi aliyejari uhuru na kujitegemea dhidi ya ugaidi
na umwagaji damu, haki dhidi ya udhalimu, Amani dhidi ya vita. Mwandishi mmoja
alisema kuwa, ‘’Vile Tanzania leo hii inapoamua kuchukua muda kuyafikiria
matakwa ama mapendekezo ya kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki, inapaswa
iangaliwe historia pia, ni jinsi gani Tanzania ililipa bei ya kuweka matarajio
yake yote mezani na kujikuta ikifanya mambo mengi peke yake ikiwemo vita ya
Kagera’’
Anaandika Daniel G. Acheson-Brown
katika tahariri yake katika kitivo cha Sayansi ya Kisiasa, Chuo kikuu cha Eastern
New Mexico na kuuliza swali “Uvamizi wa Tanzania nchini Uganda: Je ni vita ya
haki?
Nanukuu:
“Matumizi ya nguvu ya kijeshi ili
kufikia malengo ya ukombozi wa binadamu kwa mwavuli wa sababu za haki yamekuwa
ni mada yenye mguso sana tangu kipindi cha baada ya vita baridi. Hata hivyo,
miaka kabla ya kuisha kwa vita baridi, Tanzania sio tu iliichapa Uganda na
kurudisha ardhi iliyotekwa, bali iliendelea mpaka Uganda na kuung’a madarakani
uongozi wa Amini. Lakini cha kushangaza, raisi Nyerere alikuwa kwenye njia
panda tofauti sana na ile ya viongozi wa Ulaya na Marekani katika vita ya
Ghuba, yaani kwamba, je? Kuacha vita baada ya malengo yaliyopangwa ya
operesheni kutimia (Kama ilivyokuwa malengo ya kuiomboa Kagera), ama kuendeleza
operesheni mbele zaidi na kumng’oa kiongozi dhalimu? Na kwa sababu Nyerere
aliamua kuendelea na kumng’oa kiongozi dhalimu, ilimpasa pia afikirie maamuzi
yake katika kuijenga upya Uganda na sehemu yake ya uongozi, kwani msingi wa
kutumia nguvu ya jeshi kwa matumizi ya ukombozi wa watu, umesimikwa kwenye
maadili’’
Email: gabby.munyaga@gmail.com
Facebook: Gabriel Munyaga
Twitter: GabrielMunyaga
Blog: gabbymunyaga.blogspot.com
No comments:
Post a Comment